Breaking News
recent

Makonda atumia dakika 90 kutaja mafanikio 10, ahadi 10


Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda jana aliadhimisha
mwaka wake mmoja tangu ateuliwe
kushika wadhifa huo huku akitumia
dakika 90 (saa 1:30) kueleza mambo 10
aliyoyafanya katika kipindi hicho na
mengine 10 atakayoyafanya katika
mwaka wake wa pili unaoanza leo.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika
Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay na
kuhudhuriwa na wadau mbalimbali
wanaoshiriki katika vita ya dawa za
kulevya ambayo aliianzisha mapema
mwaka huu alisema amepitia
changamoto nyingi ndani ya mwaka huo
mmoja na mambo hayo yamemfanya
kuwa imara zaidi.
Alisema ataanza mwaka wake wa pili
kwa kasi mara mbili zaidi ya ile
aliyokuwa nayo katika mwaka wake wa
kwanza na kwamba atahakikisha
anafanya yale yote yatakayoboresha
maisha ya wakazi wa Dar es Salaam
sambamba na kumsaidia Rais John
Magufuli kutekeleza ilani ya CCM.
“Sasa nimekomaa zaidi na ninazo mbinu
za kupambana. Katika mwaka wangu wa
pili, nitakwenda kwa ‘speed’ (kasi) mara
mbili zaidi katika kuleta maendeleo na
kutekeleza ahadi za zilizo kwenye ilani
ya uchaguzi ya CCM,” alisema Makonda.
Mafanikio 10
Mkuu huyo wa mkoa alibainisha mambo
aliyoyafanya ndani ya mwaka huo
mmoja kuwa ni pamoja na kuendesha
kampeni ya “mti wangu”
inayohamasisha upandaji miti, ujenzi
wa wodi za wagonjwa, vita dhidi ya
dawa za kulevya na kutatua migogoro ya
ardhi kwa wananchi.
Mambo mengine aliyoyafanya ni ujenzi
wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), kampeni
ya kuchangia damu, utengenezaji wa
madawati kwa ajili ya shule za umma,
uhakiki wa silaha, usafi wa jiji na kupiga
marufuku matumizi ya shisha.
“Katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo, nilishirikisha
wadau mbalimbali kwenye kila kampeni
niliyoianzisha. Ninawashukuru wote
kwa kuunga mkono jitihada zangu,”
alisema Makonda.
Ahadi 10
Mbali na mambo hayo aliyoyafanya,
Makonda alibainisha pia mambo
mengine 10 atakayoyafanya katika
mwaka wake wa pili wa uongozi akianza
na kusimamia watumishi wa umma
kutekeleza wajibu wao katika ngazi ya
Serikali za Mitaa mpaka ngazi ya mkoa.
Alisema baadhi ya watendaji wa Serikali
wamekuwa wakisababisha usumbufu
kwa wananchi wakati wanalipwa fedha
za kutekeleza majukumu yao. Alisisitiza
kwamba katika mwaka wake wa pili,
atahakikisha kila mtendaji anatimiza
wajibu wake.
“Nitapita kuanzia ngazi ya Serikali za
Mtaa na kila mtendaji atanieleza namna
anavyowahudumia wananchi. Wananchi
wanakuja mpaka ofisi ya mkuu wa mkoa
kuleta kero zao wakati zinaweza
kutatuliwa kwenye mitaa yao, hatuwezi
kwenda namna hiyo,” alisema.
Makonda ambaye amejipatia umaarufu
zaidi kutokana na vita dhidi ya dawa za
kulevya alisema atahakikisha kwamba
anawahudumia waathirika wa dawa
hizo kwa kuwapatia tiba ya uraibu wao.
Alisema tayari amepata ardhi ya ekari
tatu aliyopewa na Azim Dewji ambayo
ataitumia kujenga kituo cha waathirika
wa dawa za kulevya ili wapate matibabu
yote wakiwa kituoni hapo badala ya
kurudi mtaani.
“Waathirika wa dawa za kulevya
wakipatiwa matibabu na kurudi mtaani,
wengi wao wanarudi kutumia dawa
hizo. Nitajenga kituo cha waathirika ili
wapate matibabu na kukaa hapohapo
kituoni.”
Kuhusu wakazi wa mabondeni, Makonda
alisema atahakikisha wote wanaoishi
katika maeneo hayo wanahama na
tayari ameagiza nyumba zao
kubomolewa kwa ajili ya kulinda
usalama wao.
Alisema wakazi waliopewa viwanja
katika maeneo hayo ambao wana hati za
viwanja hivyo, atawapatia ardhi sehemu
nyingine kwa sababu ni uzembe wa
watendaji wa Serikali na kusisitiza
kwamba watakaobainika kuhusika na
uzembe huo watawajibishwa.
Makonda alisema Mkoa wa Dar es
Salaam una maduka ya kubadilisha
fedha (Bureau de Change) zaidi ya 300
na kwamba utiriri huo umesababisha
baadhi ya wamiliki wake kujihusisha na
utakatishaji wa fedha kupitia biashara
hiyo dawa za kulevya.
“Tumewasiliana na Wizara ya Fedha
kuhusu hizo bureau na wakati wowote
wataanza kufanya uhakiki wa maduka
hayo. Hatuwezi kuwa na utitiri wa
bureau zaidi ya hata vibanda vya kuuzia
vocha,” alisema.
Mambo mengine aliyoahidi ni pamoja
na kuanzisha mfumo wa pamoja wa
ukusanyaji wa mapato, kuwawajibisha
makandarasi wazembe, kutenga eneo
maalumu kwa ajili ya kuuzia magari na
maeneo ya masoko na kuanzisha kadi
maalumu kwa ajili ya ununuzi badala ya
kuwa na fedha taslimu.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Simon Sirro alisema
mapambano dhidi ya dawa za kulevya
yanakwenda vizuri na kwamba taarifa
alizonazo zimepanda bei kwa sababu
zimekuwa adimu.
“Kupanda kwa bei za dawa za kulevya
huko mtaani kunaashiria kwamba
supply (usambazaji) ni ndogo.
Tutaendelea kupambana mpaka
kutokomeza kabisa matumizi na
biashara ya mihadarati katika mkoa
wetu na Tanzania kwa ujumla,” alisema
Sirro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya
Mkoa, Alhad Mussa Salum aliwataka
vijana kujiepusha na dawa za kulevya
kwa sababu wanapoteza utu wao na
kuwa watu wasiofaa katika familia zao
na jamii kwa ujumla.

No comments:


Powered by Blogger.