SPORTS EXTRA | ARSENAL FC: TUNASUBIRI MAJIBU YA VIPIMO VYA MRI
Klabu ya Arsenal inasubiri majibu ya vipimo vya MRI alivyofanyiwa beki wa pembeni Hector Bellerin, baada ya kugongana na Marcos Alonso wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
Bellerin, aligongwa sehemu za kichwani na Alonso alipokua kwenye harakati za kutaka kuokoa kwa kichwa mpira uliokua langoni mwa Arsenal, lakini ilishindikana na kuruhusu Chelsea kufunga bao la kwanza.
Alonso alionekana katika picha za marudio za televisheni, akimgonga kwa kiwiko beki huyo wa pembeni kutoka nchini Hispania, jambo ambalo lilizua tafrani miongoni mwa mashabiki ambao walionyesha kuvutana kuhusu uhalali wa bao la kwanza la Chelsea.
Arsenal wamedhamiria kujua ukweli wa ukubwa wa jeraha ya beki huyo mwenye umri wa miaka 21, ili kutambua itamchukua muda gani kurejea tena uwanjani.
Hata hivyo taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London imeeleza kuwa, Bellerin hatoweza kurejea mazoezini mapema, japo majibu sahihi ya vipimo vyake hayajapatikana.
Arsenal walipoteza mchezo wao dhidi ya Chelsea mwishoni mwa juma lililopita kwa kukubali kufungwa mabao matatu kwa moja, na mwishoni mwa juma hili watacheza dhidi ya Hull City kwenye uwanja wa Emirates.
No comments: