MAKALA | Salama Jabir: Mkongwe kwenye TV asiyeishiwa ubunifu
Si utamaduni wetu kusifia watu wanaoendelea kuishi. Mara nyingi tunasubiri mpaka watoweke duniani ndo tuseme Yale mazuri waliyowahi kuyafanya. Bahati mbaya wanakuwa hawana uwezo wa kusikia. Nachukua fursa hii kuzimwaga sifa zangu kwa Bi Salama Zalhata Jabir.
Alizaliwa Oktaba 1, miaka kadhaa iliyopita. Ni mwanamke mrembo, mwenye rangi ya mtume, mikato fulani hivi ya kinyamwezi. Mfupi kwa umbo, lakini mwenye akili na ubunifu mithili ya Hasheem Thabeert. Ana sauti fulani hivi yenye kukushawishi kumsikiliza hata kama anaongea nini kitasound poa tu.
Ni mtangazaji wa kike ambaye asilimia kubwa ya watangazaji waliojikita kwenye vipindi vya burudani ama walishawishika kuingia kwa kumuona mbele ya televisheni zao akifanya yake au walianza kufanya ili wawe kama yeye. Waulize watakwambia na hata wasiposema mioyo na nafsi zao zitakiri juu ya hilo!
Hapa namzungumzia yule mwanadada tuliyekuwa tukimtizama kila wiki akichambua video za wasanii mbalimbali wa kibongo na akionyesha wazi wazi hisia zake pasipo kujali matokeo ya yeye kusema hivyo. Yule mwanadada aliyejiongezea maadui kwa kusema ukweli pasi kupepesa macho yake kwa wahusika.
Kama umesahau basi kumbuka yule jaji wa moja kati ya mashindano maarufu kabisa ya kutafuta vipaji BSS ambaye kila mtazamaji na washirika husubiri aseme yeye kujua kama yaliyomo yamo? Ndiyo yule jaji ambaye haoni ubaya kuishi katika dunia yake mwenyewe ila tu aseme lile ambalo nafsi na akili yake imeona!
Sifa na utukufu zimwendee maulana kwa kutupa Salama Jabir. Kila anapokuwepo Salama basi hapana shaka unategemea burudani isiyo kifani, unategemea kupata vitu ambavyo si rahisi kupata sehemu nyingine yoyote. Kila anachokianzisha hubaki kuwa ni habari ya mjini, kuanzia Planet Bongo, BSS, Mkasi mpaka sasa Ngaz kwa Ngaz kwanini tusimpe sifa zake mwanadada?
Naamini maulana alimpa alichompa,lakini ubunifu,kutoridhika,kujituma na kupenda kuthubutu kumemweka pahala alipo. Watu wa tasnia ya burudani hasa watangazaji wa kike,mna mengi ya kujifunza kutoka kwa Salama, japo haiwezekani kuwa kama yeye, ila inawezekana kujifunza kutoka kwake na kujiongezea madini.
Na Eliezer Gibson
Instagram @gibson_elly
Instagram @gibson_elly
No comments: