Video mpya za Diamond zinavyopigana vikumbo YouTube
Jumatano hii Diamond amewashtua mashabiki wake kwa kuachia kazi zake mbili mpya ambazo zinazidi kuonyesha uwezo wake mkubwa alionao. Japo ‘I Miss You’ ni wimbo ambao ulishasikika masikioni mwa mashabiki zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini video yake imekuwa mpya machoni.
Kitu ambacho mashabiki hawakutegemea kwa sasa kuisikia sauti ya malkia wa lebo ya Mavin Records kutoka Nigeria, Tiwa Savage. Siyo kama haiwezekani lakini ni kitu ambacho kimekuwa siri zaidi tofauti na kolabo ambazo amewahi kuzifanya ikiwemo ya P-Square, Ne-Yo na nyinginezo ambapo wasanii aliowashirikisha waliweza kufahamika mapema kabla ya wimbo kutoka.
Hongera kwa Diamond kutokana na uwekezaji mkubwa anaozidi kuufanya kwenye video zake ndio unazidi kumuweka juu na kumtofautisha na baadhi ya wasanii wengine. Lakini kitu cha kushangaza kwenye video hizo ambazo zimewekwa kwenye mtandao wa YouTube ‘I Miss You’ ndio inaonekana kufanya vizuri zaidi ya ‘Fire’ ambayo amemshirikisha Tiwa Savage.
Video ya ‘I Miss You’ mpaka sasa imeshatazamwa mara 340,968 na inashika namba moja kwenye ku-treand kupitia mtandao huo wakati ile ya ‘Fire’ imetazamwa mara 143,075, zote zikiwa zimeachiwa kwa wakati mmoja.
Kutokana na mtazamo wangu nionavyo, video ya ‘I Miss You’ imeonekana kufanya vizuri mwanzoni kutokana na wimbo huo kuwa miongoni mwa nyimbo ambazo mashabiki wamekuwa wakitamani kwa muda mrefu kuona video yake ikiwemo pamoja na ngoma nyingine kama ‘Kizaizai’, ‘Ukimuona’ na ‘Lala Salama’. Video hiyo ina nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri ndani ya Tanzania kuliko nje zaidi.
Lakini tukija kwenye Fire, ina nafasi kubwa ya kupenya na kuipiku I Miss You kwa idadi ya kutazamwa zaidi hasa nje ya Tanzania kutokana na ukubwa wa Diamond pamoja na Tiwa Savage ambaye pia tayari ameshaanza kuvuka nje ya mipaka ya Afrika.
Wimbo huo unaweza ukawa mkubwa kama ilivyotokea kwenye wimbo wa ‘Kidogo’ ambao Diamond amewashirikisha P-Square, hakika Diamond mwenyewe amewahi kukiri kuwa wimbo huo ndio umempatia baadhi ya michongo mikubwa ambayo ameweza kuipata pamoja na kupenya mpaka katika baadhi ya nchi ambazo muziki wake haujawahi kufika ikiwemo kuingia kwenye playlist ya kituo cha redio cha BBC Radio 1Xtra cha nchini Uingereza.
No comments: