SPORTS EXTRA | Matumizi sahihi ya Uwanja wa Taifa yataamua hatma yetu kuelekea kufuzu AFCON 2019
Tumeshafuzu! Tumeshafuzu! Tumeshafuzu!, Hizi ni aina ya kelele ninazozisikia kwa siku za hivi karibuni tangu kutangazwa kwa makundi ya kufuzu fainali za AFCON kwa mwaka 2019 huko nchini Cameroon ambapo timu yetu tukufu ya Tanzania, Taifa Stars imepangwa kundi L sambamba na timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho.
Linaonekana kama kundi jepesi mbele ya macho ya watu wengi kwasababu hakuna timu zenye majina makubwa tuliyoyazoea kupangwa nayo kama vile Cameroon, Algeria au Ivory Coast. Mimi binafsi siwezi kukubaliana au kubishana na wadau hao lakini kuna swali moja limenijia kichwani haraka sana kabla ya kuamua upande wa kushabikia katika mdahalo huu wa kufuzu.
Tumeomba ridhaa ya Uwanja wa Taifa kabla hatujaanza kupanga mabegi yetu ya nguo kuianza safari ya Cameroon? Hili ndio swali ninalojiuliza. Lakini kuna hoja nzito sana juu ya sababu ya kujiuliza swali hili. Ebu twende sambamba nikujuze.
Septemba 8, 2007, ni siku ambayo ilikuwa inakaribia kurejesha matumaini makubwa kwenye soka la Tanzania ambapo timu ya taifa, Taifa Stars ilikuwa ikisaka pointi tatu tu mbele ya Msumbuji ili iweze kujihakikishia nafasi ya kufuzu AFCON kule nchini Ghana baada ya miaka 27 ya njaa na misukosuko kupita. Stars ilikuwa imeshajikusanyia pointi 8 kibindoni baada ya kumchapa Burkina Faso jijini Ouagadougou sawa na waliokuwa vinara wa kundi hilo, Senegal.
Stars ya Mbrazil Marcio Maximo ikiwa imesheheni wachezaji kama vile Nizar Khalfan, Abdi Kassim wenyewe wakimuita Ballack wa Unguja, Erasto Nyoni, Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Mecky Maxime na wengine wengi, waliweza kuiteka Tanzania kwa muda tu na mapenzi ya ghafla ya watu yalirudi kwa timu yao ya taifa.
Ikiwa ni mechi ya pili kuchezwa kwenye uwanja mpya kabisa wa Taifa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 tena majira ya usiku wakati taa lukuki zikimulika, watanzania walikuwa wakiamini kwamba tunampiga Msumbiji na kufuzu kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, hivyo wengi tulifurika tukiamini tushashinda.
Watanzania wote tuliokuwa tukiitazama mechi ile LIVE kutokea uwanjani na wale tuliokuwa tukiangalia kupitia TV tulishuhudia jinsi Tico Tico alivyotunyamazisha kimya dakika ya nane tu kwa kichwa cha kuchumpa, na baada ya hapo tukaanza kuwa watumwa wa kulisaka goli la kusawazisha na hatimaye la ushindi na hadi dakika 90 zinakamilika hakuna tulichopata licha ya mashuti kadhaa ya Abdi Kassim kumsumbua golikipa wa Msumbiji. Ndoto tulizoanza kuziota zilizima ghafla na wenye kulia walilia lakini tuliondoka na somo kubwa sana. Tuachane na Tico Tico…
Miaka takribani miwili mbeleni tulikuwa kwenye kundi “jepesi” katika harakati za kufuzu fainali za Kombe la dunia kwa mwaka 2010 ambapo tulipangwa na vibonde Cape Verde na Mauritius huku mbabe Cameroon peke yake ndiye alionekana kutuumiza vichwa. Kila mtu alishangilia akiamini tunaweza kupata nafasi ya pili na kufuzu kama ‘Best looser’ kuingia raundi inayofuata maana tuliamini tutawapiga vibonde hao wawili nje ndani na kufikisha alama 12 kabla hata ya kukutana na Cameroon.
Tulikuwa na nafasi ya kuanza vizuri lakini kinyume na matarajio ya wengi tuliishia kupata sare mbele ya kibonde Mauritius tena uwanja wa nyumbani huku tukilitafuta goli la kusawazisha kwa mbinde bila kusahau jinsi ambavyo Emmanuel Gabriel alikosa penati.
Baada ya mechi hiyo kuisha licha ya umri wao kuwa mdogo kipindi hicho, niliweza kujua dhahiri kuwa hatuna nafasi tena ya kufuzu na cha kushangaza Cameroon ambaye kila mmoja wetu alimuogopa, ndiye tulicheza nae kiutu uzima nusura tugawane pointi kwenye mechi zote mbili tulizokutana kama sio ukongwe wa Samuel Etoo.
Nnachojaribu kuzungumzia hapa ni matumizi ya uwanja wa nyumbani katika mechi za kimataifa na wengi wenu mtakubaliana na mimi kuwa mara nyingi safari yetu imekuwa ikiishia njiani kwasababu ya matumizi mabovu ya uwanja wa Taifa.
Waswahili tuna msemo unasema “Mcheza kwao hutunzwa”, lakini ni kweli kuwa Uwanja wa Taifa hututunza pale tunapokuwa tukiutumia? Jibu ni hapana. Kwenye makundi haya ya kufuzu ambapo huwa na timu nne, kila timu lazima icheze mechi sita ambapo tatu ni za nyumbani na tatu ni za ugenini na katika suala ambalo huwa linatushinda sisi Watanzania ni kushinda mechi zote za nyumbani hata tupangwe na timu nyepesi vipi.
Najaribu kuangalia kundi jepesi tulilopangwa kwenye kufuzu Kombe la dunia mwaka 2010 ambapo hatukuwa na sababu ya kushindwa kuwafunga Mauritius nyumbani na hata Cameroon pia licha ya jina lao kubwa na badala yake tukaishia kupata sare wakati tulikuwa na uwezo wa kupata ponti zote tisa za nyumbani pamoja na zile za Mauritius tulizozipata ugenini ili kuwa 12.
Tulifanya masihara mechi dhidi ya Mauritius halafu tukaja kukaza mechi dhidi ya Cameroon. Kwahiyo utaona jinsi ambavyo tunavyodharau baadhi ya mechi na kuzipa umuhimu nyingine na kukumbuka mashuka kukiwa kumekucha.
Ni kweli kundi hili tulilopangwa kwa sasa tukiwa na Uganda, Cape Verde na Lesotho linaweza kuwa kundi jepesi machoni, lakini sio kiuhalisia.
Tunawazungumzia Uganda ambao wamefuzu AFCON mwaka huu huku miaka ya hivi karibuni wakiwa wametugeuza vibonde wao nje ndani. Unaizungumzia Cape Verde ambao wameshatuacha mbali wakiwa sio wale tuliokuwa nao kundi moja mwaka 2007 kwani wenzetu miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakifuzu AFCON mara kwa mara, huku nikikumbuka jinsi ambavyo Lesotho walitufunga mwaka 2015 kwenye kombe la COSAFA kimzaha mzaha. Sasa tuna ujasiri gani wa kusema ni kundi jepesi?
Sisemi kwamba hatuwezi kufuzu, lakini ninachojaribu kukumbusha ni kwamba matumizi ya uwanja wa nyumbani ni muhimu sana kwenye mechi za aina hii. Ni lazima tujiwekee mipango ya awali ya kushinda mechi zote tatu za nyumbani kisha ndio tuanze kupigia mahesabu ya kumfunga mtu kwao au kutoa sare.
Anachotakiwa kufanya Salum Mayanga ni kuhakikisha kila mechi ya nyumbani kwenye kundi hilo anaichukulia kwa uzito mkubwa huku akiwaandaa vijana wake kisaikolojia kupambana haswa bila ya kuruhusu mgeni kuondoka na alama yoyote kutoka Uwanja wa Taifa.
Anachotakiwa kufanya Salum Mayanga ni kuhakikisha kila mechi ya nyumbani kwenye kundi hilo anaichukulia kwa uzito mkubwa huku akiwaandaa vijana wake kisaikolojia kupambana haswa bila ya kuruhusu mgeni kuondoka na alama yoyote kutoka Uwanja wa Taifa.
Na sisi pia mashabiki tuhakikishe tunaitumia vyema fursa ya nyumbani kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuishangilia timu yetu ili inyakue alama tatu muhimu nyumbani. Tunaweza kufuzu kwenda Cameroon endapo tu tutaomba ridhaa ya Uwanja wa Taifa. Ridhaa hii si nyingine bali ni kutumia vyema uwanja huo kupata matokeo na sio kukaa na kujipa moyo kuwa tutafuzu kiulaini wakati wachezaji wetu hawana hamasa wanapocheza nyumbani huku wengine tukiwa ndio vinara wa kuwazomea wachezaji wetu wanapokosea.
Licha ya ubora wa kikosi kuwa ndio silaha pekee ya kufuzu lakini uwanja wa nyumbani ni silaha muhimu sana katika harakati za kufuzu. Ni vyema tujifunze kutoka kwa wenzetu jinsi wanavyotumia vyema viwanja vyao vya nyumbani kwasababu kama tuliweza kutoka sare na Cameroon enzi hizo basi hatushindwi kumfunga Uganda kama tukitumia nguvu na hamasa ile ile tuliyotumia.
No comments: